Saturday, 26 September 2009

Tujifunze kwa mfano wa Yona

WARAKA KWA WAJUMBE WA MKUTANO MKUU KKKT - DKK 10/2007

TUJIFUNZE KWA MFANO WA YONA


Ndugu wajumbe nawasalimu katika jina la YESU kristo Bwana na Mwokozi wetu. Ni matumaini yangu kuwa utakuwa bado umefunikwa na damu ya Kristo.

Ndugu wajumbe ni mara yangu ya kwanza kabisa kuwaletea waraka kama huu. Lakini nimeshawatumia nyaraka nyingine kama hizi wajumbe wa Halmashauri kuu.

Nia na madhumuni ya kuandika Nyaraka hizi ni kujaribu kutoa picha kuhusu masuala ya kiuongozi, kiutawala na kiutendaji ambavyo yamechangia kukua au kushuka kwa imani ya kiroho kwa washarika wetu na ustawi wa kanisa letu.

Kanisa ni mwili na Kristo ni kichwa, ni wajibu wa mwili kufuata maelekezo ya kichwa. Lakini mwili unaviungo mbali mbali hivyo basi inaweza tokea kiungo kimoja, tuseme, kwa mfano Ulimi ukaponyoka na kuongoza upotevuni. Na kama viungo vingine havitawasiliana kuona kuwa ulimi hauendelei kwenda upotevuni basi mwili wote hupotea.

Madhumuni ya waraka wa leo ni kushiriki pamoja nanyi katika mifano michache ambayo inatoka katika Biblia ambayo nimeisikia kwa nyakati tofauti toka kwa Wanatheolojia maarufu wa DKK, wachungaji wanaoheshimika sana kwa mafundisho.

Kwa karibu kwa kipindi cha miaka minne ya mwisho Dayosisi yetu imejikuta katika matatizo makubwa ya kiutawala. Matatizo ambayo yametokana na udhaifu wa ujuzi wa utawala wa viongozi wetu na usimamizi mbovu wa mali na fedha za dayosisi[1].

Jambo la kusikitisha hasa kwa sisi wadau ambao tuna sera na fikra mbadala ni kuwa hatuoni jitihada zinafanywa au kuchukuliwa ili kutokomeza tatizo hilo.

Ukaguzi wa fedha wa mwaka 2006 uliofanywa na wakaguzi toka makao makuu ya kanisa KKKT – Arusha ulibaini wizi wa zaidi ya Milioni Ishirini. Wizi huu ni ule uliotokea katika kitengo kimoja tu cha hospitali yetu ya Bulongwa hili limetokea miaka mitatu baada ya Dr. Mpumilwa kuondoka. Hatua zilizochukuliwa ni kumwondoa aliyekuwa Mhazini mkuu wa Hospitali. Je inatosha? Sasa hivi kuna kiasi kikubwa cha mbao kinatolewa kila siku hapa hospitali, hakuna anayejua kiasi cha mbao wala mapato yake yanaenda wapi?

Baba Askofu Shadrack Manyiewa akihubiri katika ibada ya siku ya Tamasha la Uimbaji kidayosisi pale usharika wa Iniho jimbo la Magharibi, alisema Rushwa (Fedha) imesabisha watu kupotosha ukweli.
Katika tamasha hilohilo kwaya ya Upendo ya jimbo la kati katika wimbo wa utamaduni uliokuwa na mahadhi ya asili ya kihehe au kibena kama sijakosea, waliimba kuwa Rushwa imeingia mpaka kanisani. Kama mtazamo wa Baba Askofu na waimbaji hao ni sahihi, hii inamaanisha kuwa, hata kanisani ukweli umepotoshwa kutokana na pesa na rushwa.

Na kama hatutachukua hatua kutatua tatizo la rushwa ndani ya kanisa basi tusitegemee haki kutendeka wala kujua ukweli kwa yale yanayoendelea ndani ya kanisa letu.

Katika mkutano mkuu maalum ulifanyika mwaka 2006, Baba Askofu Shadrack Manyiewa alisema, “mgogoro wa Dayosisi na shirika la PIUMA ulianza wakati vikao vya dayosisi vilikuwa vinazungumzia ripoti ya ukaguzi kuhusu ubadhirifu wa fedha. Na kisha vikao hivyo kuamua hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi ya wahusika. Kabla hatua hazijachukuliwa PIUMA iliamua kutangaza ripoti hiyo katika vyombo vya habar”i. Alizidi kusema, “pia PIUMA waliendelea kuchimbua mambo ya dayosisi na kuwatumia waandishi wa habari kutafuta mapungufu na madhaifu ya uongozi wa kanisa ili kuutangaza hadharani na kufanya maandamano”.[2]

Katika taarifa hii iliyotolewa na Baba Askofu, anasema kuwa wakati mgogoro na PIUMA unaanza mwaka 2006 mwezi Machi, vikao vya dayosisi vilikuwa vinakaa kuangalia hatua za kuchukua dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuwa wamekula fedha ya kanisa. Sasa sisi tunajiuliza kuwa sasa ni mwaka mmoja na nusu toka Machi 2006 na mwaka mmoja kamili toka Oktoba 2006 hotuba ya Baba Askofu ilipotolewa. Je vikao hivi vya dayosisi vinaendelea kukaa ili viweze kutuambia washarika ukweli juu ya kilichotokea katika sakata hili la ubadhirifu wa pesa?

Hapa ndipo neno la Baba Askofu Manyiewa, kuwa Pesa zimesababisha watu kupotosha ukweli, linaponikolea. Nakubaliana naye Mia kwa mia. Kama sio pesa ni nini? Nani huyu anayeficha ukweli wa ubadhirifu huu na ambaye hataki hatua za kisheria zichukuliwe? Bila shaka ni mtu mwenye pesa tena mwenye pesa nyingi sana kuliko wachungaji wetu wa sharika za Kijiombo na Unenamwa. Na lazima awe na nguvu ya kuvifanya vikao vya Dayosisi vinavyotajwa na Baba Askofu kuogopa kutoa hadharani taarifa ya wakaguzi au hata kufikia maamuzi ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuiba pesa hiyo.

Hili ni tatizo la kiuungozi katika kipengere cha utawala. Nani anatakiwa kusimamia zoezi hili ili haki itendeke? Bila shaka ni Halmshauri kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu. Makatibu wakuu mbali mbali tofauti wameshindwa kuiongoza Halamshauri kuu kwasababu, halmashauri kuu yetu imekuwa mara kwa mara na migogoro na Makatibu wakuu.

Juzi tumesikia habari za kujiuzuru kwa Katibu mkuu mpya aliyekuwa ameteuliwa kama miezi miwili tu iliyopita. Huyu atakuwa ni Katibu mkuu wa saba katika kipindi cha miaka nane tu. Hii inamaanisha kuwa kwa wastani tumekuwa na Katibu mkuu mpya kila mwaka mmoja.

Mimi siamini kuwa Makatibu wakuu hawa wote Saba wameshindwa kazi, au walishindwa kuwa na taaluma za kimenejimenti. Lakini nadhani kuna tatizo kubwa zaidi linalowafanya washindwe kabisa kufanya kazi zao kwa uhakika.

Mathalani habari tulizozipata toka ndani ya watu waliokaribu kabisa na kamati ya Utendaji ya dayosisi iliyokutana kujadili suala la kujiuzuru kwa Katibu Mkuu mpya zinatueleza kuwa, Katibu Mkuu mpya alishindwa kuvumilia baada ya kuona kuwa nafasi yake haitambuliwi na wala hakupewa nafasi ya kuonyesha utalaam na ujuzi wake. Kwa ujumla hakupewa ushirikiano.

Inasemekana kuwa kumekuwepo na mwingiliano na mgongano wa kazi na madaraka kati ya viongozi wetu wakuu yaani wale waliopewa dhamana ya kuwa viongozi wa kufundisha neno la Mungu pamoja na kuongoza mambo yote ya kiroho (Katiba Kanuni X A1,Sheria IX) na wale ambao wanasemwa na katiba kuwa watasimamia ofisi ya Dayosisi na kuwa watendaji wakuu (Katiba X C1,Sheria XI)[3]

Mathalani ni matumaini yetu kuwa mali za dayosisi kama vile magari zinapouzwa Katibu Mkuu na kamati ya fedha watashirikishwa katika zoezi lote. Lakini cha kushangaza ni kuwa dayosisi yetu iliuza Landcruiser Hard top, kamati ya fedha wala Katibu Mkuu hawakuwahi kushirikishwa katika mpango wa kuuza gari hilo.

Swali gumu zaidi ni kuwa mpaka tunapochapa barua hii, fedha zimeshatumika, halmashauri haijasomewa matumizi ya fedha hizo. (Na hapo kuna msimamizi wa fedha na mali toka Makao makuu ya kanisa,hali itakuawaje atakapoondoka?). Wajumbe wa mkutano mkuu huu ni matumaini yetu kuwa watapewa taarifa ya fedha watakayoipitia msitari baada ya msitari. Waweze kufahamishwa kwa undani juu ya matumizi ya fedha hii. Inasadikika na wengi wetu wanajua jinsi pesa hii ilivyotumika. Maofisa wetu wamegawana wengine sh.3,600,000- wengine wamepata sh.1,500,000- haya yanafahamika ila “Rushwa imepotosha ukweli”, watu hawataki kusema ukweli!!!

Haya yote yametokea bila Katibu Mkuu kujua wala kushirikishwa kwa namna yoyote ile.

Baada ya mauzo na mgao wa pesa hizo, sasa sikiliza nikupe tofauti nyingine, hivi karibuni kulikuwa na semina ya wachungaji wetu pale Tandala, semina iliyoandaliwa na Idara yetu ya Udiakonia. Udiakonia walikuwa na jukumu la kutunza na kulisha watumishi wa Bwana waliofika katika semina ile, wala haikuwa kazi ya Head Office kutoa takrima kwa wanasemina hao. Udiakonia walitimiza wajibu huu vizuri pasi malalamiko wala manung’ukuniko toka kwa wachunga kondoo waliohudhuria semina hii.

Cha kushangaza ni kuwa jioni moja wachungaji waliokuwa wakihudhuria semina walijikuta wakikabidhiwa bahasha yenye kitita cha shilingi elfu tano kila mmoja. Katibu Mkuu mteule inasemekana alishangaa kwa maana hakujua kama kuna fungu lolote la pesa lililopangwa toka ofisi yake kutumika kwa kazi hiyo,inasemekana hakusita kuuliza kuwa pesa hizo zimetoka wapi? Alipewa jibu kuwa zimetolewa na Head office.

Kiutaratibu matumizi ya pesa head office kwa mujibu wa kanuni za fedha za kanisa (ELCT Financial Regulations na ELCT Accounting Manual) zinaeleza kuwa pesa ya dayosisi kabla ya matumizi lazima ziidhinishwe na Katibu Mkuu, na si vinginevyo. Habari za Uhakika tulizonazo zinasema kuwa jumla ya shilingi laki tano (500,000-) zilitolewa kwa wachungaji hao. Sasa tunajiuliza ilikuwaje Pesa hii ilitolewa bila Katibu Mkuu kushirikishwa au kujua? Hapa kuna njama za makusudi za kuingilia kazi za watu, au kuna kiongozi asiyejua wajibu wake. Na huyu ndiye chanzo cha matatizo haya yote.

Kabla hilo halijaisha tunaambiwa kuwa wafadhiri wamezidi kuibana dayosisi yetu, wakitaka kujua namna pesa zao walizotuma katika vipindi mbali mbali zilivyotumika. Uongozi wa dayosisi bila kumshirikisha Katibu Mkuu mpya, uliamua kuunda tume itakayo pita katika kila sharika zinazopokea pesa toka nje kujua zilitumikaje.

Watu wananong’ona kuwa kazi ya tume hiyo ilikuwa ni kubaini pia kama kuna chenji imebaki ili irudishwe makao makuu ya dayosisi hata kama pesa hizo zilitumwa moja kwa moja na wafadhiri kwenda kwenye sharika.

Kikatiba na kiutendaji ni kazi ya Katibu Mkuu akishirikiana na Halmashauri kuu kuunda tume kwa maswala kama haya yanapojitokeza. Lakini la kutushangaza sisi sote ni kuwa wakati tume hii imeshaanza kazi (ilipata shida pale Madihani) ndipo Katibu Mkuu anapata barua toka kwa Baba Askofu kuwa anaombwa kushirikiana na tume iliyoundwa.

Sasa atashirikiana vipi na tume wakati wa uundwaji wake hakufahamishwa wala kushirikishwa? Sababu zote hizi pamoja na nyingine nyingi ambazo hatujapata nafasi ya kuziandika zote katika waraka huu, zilimfanya Katibu Mkuu huyo mpya kujisikia mnyonge na asiye na nguvu wala thamani mbele ya maofisa wenzake wa dayosisi na mwisho wake alilazimika kujiuzuru.

Baada ya Tume hiyo iliyoundwa kinyume cha utaratibu kushindwa kufanya kazi iliyopewa ya kusafisha jina la ofisa wetu, baada ya ujanja huu kugunduliwa na washarika mbali mbali. Inasemekana taarifa isiyokuwa ya kweli, tunaweza kuiita ya kugushi imetengezwa ili kuipeleka kwa wafadhiri. Taarifa za ndani kabisa toka idara ya hazina zinasema taarifa hii haina sahihi ya Katibu Mkuu. Katibu mkuu alishindwa kutia sahihi katika makaratasi hayo kwa sababu taarifa hii ilikuwa imebeba taarifa nyingi zisizo sahihi.

Wafanyakazi wa ndani wa dayosisi hasa makao makuu wanasema kuwa hata wakati ambapo viongozi wa juu wanapotaka kumwagiza kitu Katibu Mkuu walikuwa wakimwita Kaimu Katibu mkuu msaidizi na kumpa maelekezo yanayohusu ofisi ya Katibu Mkuu. Kaimu Msaidizi wa Katibu Mkuu ndipo anapoenda kumwelekeza bosi wake Katibu Mkuu, kuwa Baba anasema hivi na hivi, au ufanye lile na lile. Hili kiutawala ni uvunjifu wa itifaki, hii inawezekan tu kama anayehusika ni monita wa Darasa la tatu, lakini sio viongozi wa juu wa dayosisi. Kosa kam hili linaashiriwa udhaifu wa mkuu katika taaluma ya utawala.

Sasa ndugu yangu mjumbe hata kama ungekuwa wewe ndiye katibu mkuu kwa sababu kama hizi ungevumilia? La HASHA! Kwa hiyo kuna tatizo zaidi ya upeo wetu wa kuona kwa macho kwamba Makatibu Wakuu ndio wakorofi.

Bahati nzuri sana tumeshawahi kuwa na Makatibu wakuu ambao hawakupenda rushwa wala ubadhilifu ndani ya kanisa. Makatibu wakuu hawa walitenda kazi zao kwa uadilifu, lakini bahati mbaya sana maofisa wenzao walihakikisha kuwa wanawafanya wachanganyikiwe na kuichukia kazi yao.

Mwisho wa yote walibambikiwa tuhuma za mambo ambayo hawakuwahi kuyatenda na Halmshauri kuu yetu ilitumika katika kupitisha maamuzi, ya aidha kuwafuta kazi au kuwafanya wakachukia kazi zao. Mathalani kuna Katibu Mkuu mmoja aliambiwa kuwa yeye anatoa siri za Dayosisi nje na kuwapa watu ambao wanachimba madhaifu ya dayosisi. Ameondoka. Na leo tunahabari za ndani kabisa juu ya maofisa walivyogawana pesa iliyotokana na mauzo ya landcruiser. Je, na hiyo ni yeye ametupa?

Sasa hivi kuna minong’ono kuwa uongozi wa juu wa Dayosisi umekasirishwa na kitendo cha Katibu Mkuu huyu mpya Kujiuzuru, kwa hiyo kuna mpango wa kumng’oa katika nafasi yake anayoshikilia sasa ya ukuu wa shule ya Sekondari na kumpangia usharika wa Nkenja. Unadhani wakifanya hivyo watakuwa wametumia Busara! Umefika wakati wa kumpima kiongozi kwa “Tunda la Roho uvumilivu, Utu wema”

Ndugu Mjumbe,
Tatizo sio watu wala PIUMA wanaochimba habari za udhaifu na mapungufu ya uongozi wa dayosisi. Bali tatizo ni upungufu na udhaifu wa uongozi wa dayosisi wenyewe. Mapungufu hayo yanafahamika, udhaifu huo unafahamika, watu wa kurekebisha wanafahamika! “usipoziba ufa utajenga ukuta”

Tufanyaje? Ndugu Mjumbe!
Mwanatheolojia maarufu wa dayosisi yetu, ambaye alisomea theolojia katika chuo cha Moravian, Mbeya, ambaye kwa sasa ni mstaafu, siku moja wakati akihubiri katika usharika fulani uliokuwa na mgogoro wa kiuongozi, alisaidia kutatuliwa kwa tatizo kwa somo lake la siku hiyo kwa washarika wote la “Tujifunze kwa Mfano wa Yona”. (Yona, 1- 4)

1. Mwanatheolojia huyo alisema, Jambo muhimu la kwanza ni Yona kuasi na kutaka kujiepusha na uso wa Bwana. Yaani, badala ya Yona kwenda Ninawi kama alivyokuwa ametumwa na MUNGU yeye aliamua kwenda Tarshishi. Kwa hiyo ni jambo muhimu sana kutambua kuwa kuna Yona hapa aliyepokea wito wa Bwana lakini ameshindwa kuutekeleza. Ameamua kufanya yale yanayomuuzi Bwana, (kama watoto wa Eli)

2. “lakini bwana alituma upepo mkuu baharini, ikawa tufani kubwa baharini, hata merikebu ikawa karibu kuvunjika” Yona 1:4. Mpendwa mjumbe kwa miaka minne mfululizo hujaona kuwa Dayosisi yetu ni sawa na merikebu aliyokuwa amepanda Yona? Kuna tufani kubwa na merikebu inayumbayumba ikaribu kuvunjika.

3. Tukiangalia mfano wa wale mabaharia tunaona kuwa hawakukaa tu bali walichukua hatua.
· Kwanza: Biblia inatuambia, waliogopa
· Pili: kila Mtu akamwomba Mungu wake
· Tatu: wakatupa baharini shehena iliyokuwa merikebuni.

Kwa hiyo hapa tunajifunza kuwa sisi kama mabaharia na abiria katika merikebu yetu inayosongwa songwa na upepo mkali na tufani, labda hatujaogopa na kumshirikisha Mungu wetu. Hizi ni hatua kuu muhimu ambazo wakati wote tunapozungumzia maswala ya kanisa ni lazima tuzipe kipaumbele.

4. Mwanatheolojia huyo anatuambia kuwa mabaharia hao walipobaini kuwa mambo yote hayo yaliwapata kwa sababu ya Yona walitaka kujua ni mtu wa namna gani. Naye alipowaambia kuwa yeye ni mwebrania, naye anamcha BWANA, Mungu wa mbingu, aliyeziumba bahari na nchi kavu. Ndipo watu wale wakaogopa mno, kwa maana walijua yale yote yaliwapata kwa sababu Yona alikimbia ajiepushe na uso wa BWANA.

Je ndugu mjumbe umewahi kuhisi kuwa ndani ya merikebu yetu kuna Yona? Kama ndivyo au ndio unasikia sasa kwa mara ya kwanza, basi swala muhimu ni kuiga mfano wa wale mabaharia wa wakati wa Yona wa Biblia. Walimuuliza Yona wao, “wewe ni nani? Wa kabila gain? n.k, Na sisi tuchukue nafasi tumsome Yona wa kwetu, Uwezo wake wa kuongoza, uadilifu wake katika pesa na kiroho. Wenzetu wa ile merikebu iliyokuwa inaenda Tarshishi walipiga kura, sisi wa merikebu ya leo hatuna budi kufanya uamuzi sahihi, ni lazima kufikia uamuzi, tena uamuzi sahihi, sio wa kampeni au ushawishi, bali ule wa mpango sahihi wa Mungu. KURA YAKO ITAIOKOA DAYOSISI.

5. Kifungu cha kukumbuka ni kutoka katika mstari wa 12. “..Naye akawambia nikamateni, mnitupe baharini; basi bahari itatulia; maana najua ya kuwa ni kwa ajili yangu tufani hii imewapata”[4]

6. Ni wazi kuwa kuna Yona, ni kweli kuwa kwa ajili yake tufani imetupata. Lakini utofauti wa Yona wa kwetu na yule Yona wa Biblia ni kuwa Yona wa Biblia alikuwa amejitoa yeye mwenyewe kuokoa merikebu isije ikavunjika na kuwaua hata watu wengine wasio kuwa na hatia. Alitambua kosa lake na aliwambia wale mabaharia nini cha kufanya, yaani alijitoa mhanga kuwa wamtose baharini ili waweze kupona. Wakati Yona wa kwetu ameendelea kupiga filimbi na kelele za kuwa nimeonewa sio mimi.

7. Wakati Halmshauri Kuu ya dayosisi yetu inakaa kujadili suala muhimu la kuisaidia merikebu, yeye huinamisha kichwa chake na kuanza kulia kama mtoto mdogo kuomba asaidiwe “si kweli, wananionea”.

8. Ni jambo la kibinadamu kuoneana huruma, tunaambiwa kuwa hata wale mabaharia wa wakati wa Yona wa Biblia walioona huruma wakaamua kuvuta makasia kuelekea pwani. Lakini nguvu ya Bwana ikawa kubwa zaidi wasiweze. Hata sisi inawezekana kuwa tunaona shida, tufani imetusonga, lakini tunatumia akili ya kibinadamu kufikiria kufikia maamuzi haya. Tunajaribu sana kuvuta makasia kuelekea pwani lakini tunapaswa kupima nguvu ya upepo tunaoshindana nao. Mathalani kila Halmshauri kuu inapokaa tunasikia wamerekebisha hili na lile, washarika wanaanza kupata matumaini mapya, lakini baada ya siku mbili unasikia tena, lile jambo limeharibika zaidi.

9. Lakini Yona aliwasisitiza wamtupe kati kati ya bahari, kuiokoa na watu waliokuwa hawana hatia ndani ya ile merikebu, Ndipo watu wale walipomkamata Yona wakamtupa Baharini, nayo bahari ikatulia.

Mwanatheolojia huyu wakati akifundisha somo hili alisema, jambo la muhimu la kujifunza kwa moyo ni nafasi ya Yona. Kuwa, Yona wa Biblia alikuwa tayari kukubali kuwa yeye ndiye chanzo cha tatizo, na hata kujitoa kutupwa baharini. Walipomuuliza “Tukutende nini, ili bahari itulie? Hakulalama munanionea, munanionea. Alijua kuwa yeye ndiye chanzo cha tatizo, ndivyo ilivyo hata sisi mabaharia wa merikebu yetu tumwambie Yona u-mtu wa namna gani? Tumwambie mambo haya yote yanatupata kwa ajili yako.

Viongozi wanapaswa kuwa watu wasikivu wanaopenda kusikiliza yale wanayoambiwa na mkutano wanaouongoza.

Mchungaji Luhuvilo Sigalla, Msaidizi wa Askofu, mstaafu alipotembelea Lutheran Junior Seminary mwaka 1995. Katika ibada moja ya Asubuhi alifundisha Neno toka katika kitabu cha Hesabu, somo lilikuwa “kwa nini Mungu hakumruhusu Musa kuingia Nchi ya ahadi”.[5]

Leo si nia yangu kurudia sababu za kumfanya Musa asiingie nchi ya ahadi, lakini napenda tu niwashirikishe mafundisho ya Mch. Sigalla, kuwa inawezekana viongozi wetu wakawa kikwazo cha kuuona ufalme wa Mungu. Lakini wanapaswa kutambua kwa akili zao, na kwa msaada wa roho mtakatifu kuwa wao ni kikwazo na hivyo basi wafanye uamuzi wa kurekebisha maswala yaende vizuri.
Musa hali akijua kuwa hataingia nchi ya ahadi anamwandaa Yoshua[6]. Musa hapotezi muda kubishana na Bwana (kama alivyofanya Sauli alipopata habari za Daudi kuja kuwa Mfalme) bali Musa anachukua hatua ya kukubali kuwa hadi hapa nilipowafikisha wanaisrael inatosha acha mtu mwingine awavushe nchi ya ahadi.

Bado jambo la kishujaa zaidi ni Musa kwa miguu yake mwenyewe anakwea mlima Abarimu, mpaka kilima cha Nebo.[7] Huku akijua kuwa hatarudi tena chini ya mlima kuonana na watu wake aliowapenda ukomo, watu aliokuwa tayari kufa kwa ajili yao. Lakini anajua wakati umefika wa yeye kuondoka duniani. Angeliweza kumlilia BWANA na kutubu kweli kisha kumwomba Bwana kuwa amruhusu hata avuke ng’ambo, angalau akatoe Sadaka tu, Kanani kisha ndio afe. Lakini Musa ni mtiifu, anakubali kufa, ili wana wa Israel kwa msaada wa Joshua wafike nchi ya ahadi.

Kwa hiyo Wajumbe wa Mkutano Mkuu lazima tujifunze kwa mfano wa Yona na Musa, hadithi ambazo zimehubiliwa na Wachungaji wetu wa Dayosisi hii mara nyingi. Tunao akina Joshua wengi tu katika kanisa. Tuwape kazi ya kutufikisha Kanani. Tumeshafika kwenye kilele cha Nebo, tumeiona nchi ya ahadi iliyojaa asali na maziwa.

Hatuwezi kuifikia nchi hii kwa sababu ndani ya merikebu yumo YONA, na kama Yona hatajitokeza kusema ni kwa ajili yake yote haya yanatupata, sipendi niwafiche hatutafika popote. Watatudanganya kuwa si munaona walisema wazungu wameacha uhusiano na sisi, mbona wamekuja na wametununulia na Ng’ombe? Ukweli hata Yona wa Biblia wakati meli ipo katika hatari yeye alilala usingizi, unadhani kwa kulala kwake kulimaanisha hakuna hatari?

Nchi ya ahadi ipo mbele yetu, lakini ni lazima Musa akwee kilima Meliabu mpaka kilele cha mlima Nebo, maana kama ataendelea kuongoza msafara tutaendelea kuzunguka jangwani hatutaifikia nchi ya ahadi.

Hata misemo ya Kiswahili inatuelimisha namna ya kufanya tunapokuwa katika wakati kama huu, waswahili wanasema “ukicheka na Nyani Utavuna mabua” Mtoe nyani shambani kabla hajakuletea athari kubwa zaidi. Ukimwangalia usoni utaona sura ya mfano wa mtu, kwa hiyo utaona huruma, ukweli ni kuwa huwa hutumwangalii nyani usoni wakati kama ule ukifika.

Hata hivyo tuna nafasi ya kurekebisha, kwani neno linasema, “LAKINI NINALO NENO JUU YAKO KWAMBA UMEACHA UPENDO WA KWANZA KUMBUKA ULIPOANGUKIA HEBU SASA UKATUBU”

Neema ya BWANA wetu YESU Kristo na Upendo wa MUNGU Baba na ushirika wa roho mtakatifu, ukae nanyi nyote sasa mnapotafakari safari ya dayosisi yetu kuiendea nchi ya ahadi kwa kujifunza mfano wa Yona.

AMENI!

Mkereketwa wa Maendeleo Makete.
[1] Taarifa za ukaguzi wa fedha Moses AB & Comapany; certified Public Accountants in Public Practice
[2] Taarifa ya Baba Askofu kwa wajumbe wa mkutano Mkuu Maalum mwaka 2006 Bulongwa.
[3]KATIBA ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania – Dayosisi ya Kusini Kati
[4] Yona 1:12, Mh.9:18
[5] Hesabu 20:1-12, Kut. 17:1-7, 16:2,7-12
[6] Kumb 31; 14 – 16, Kumb. 4:10, Kut. 33:9
[7] Kumb 32; 48 – 52, Hes. 27:12-14, Kumb. 3:23-27